Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo kutoka kwa wafu, tupate urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.
1 Petro 1:3–4
Petro anafungua waraka wake wa kwanza kwa kutujulisha kwamba kuzaliwa upya humpa kila mwamini tumaini lililo hai kupitia ufufuo wa Bwana Yesu Kristo. Tumaini hili lililo hai linatuleta katika nini? Warumi 8:17 inatukumbusha kwamba sisi ni "warithi wa Mungu" na ukweli huu unapatikana katika Agano Jipya lote (Efe. 3:6; Tit. 3:7).
Urithi huu ambao tumeingizwa unajumuisha nini? Kwanza, unajumuisha kurudi kwa Kristo kwa ajili yetu (Yoh. 14:1–3; 1 The. 4:13–18). Unajumuisha ahadi ya ufufuo (1 Kor. 15:20–23; Flp. 3:10–11). Ahadi za uzima wa milele (Yoh. 3:16; 1 Yoh. 2:17), za thawabu ya mbinguni (2 Kor. 5:10), za pumziko la milele (Ebr. 4:1–11), na za mbingu mpya na dunia mpya (2 Pet. 3:13; Ufu. 21:1–2). Hizi ni baadhi tu ya ahadi tulizo nazo katika Kristo. Lakini tunaweza kujiuliza ahadi hizi za kile kilicho mbele zinahusianaje na maisha yetu ya sasa?
Kwa sababu mimi na wewe tumeletwa katika tumaini lililo hai, tunaweza kumwamini Baba yetu mwenye upendo katika kila hali tunayokabiliana nayo maishani. Tunajua sisi ni wake milele (Efe. 1:13–14). Kwa kuwa sisi ni wake, ataendelea kutulinda, kutupatia mahitaji na kutufanya tukue katika imani yetu, akitufanya tufanane na mfano wa Mwanawe mpendwa.
Tunaweza kupita katika maji ya kina kirefu katika maisha haya, lakini hatupaswi kusahau kamwe kwamba tumezaliwa kwa tumaini lililo hai katika Kristo, na maji haya ya kina yanaruhusiwa ili kutufanya tufanane na mfano wake (Rum. 8:28–29). Tumaini hili lililo hai si la siku ijayo tu; ni la kile ambacho huenda unapitia wakati huu!
Mtangazaji wa Leo:
Tumaini kwa Mungu!